Akiongoza kikao cha Baraza la Wafanyabiashara Wilaya ya Mbinga Mwenyekiti wa kikao hicho Mh. Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Ndg. Cosmas Nshenye aliwaeleza wajumbe wa kikao kuwa umefika wakati wa kuchangamkia fursa zilipo ili waweze kuwekeza na kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya tano kuwa na Viwanda vya kutosha.
Kikao hicho cha leo kilikuwa ni mwendelezo wa kikao cha awali kilichofanyika tarehe 24/11/2018 ambapo fursa mbalimbali za uwekezaji zilianinshwa kama vile, Uendelezaji wa Kilimo na Umwagiliaji, Mifugo na Uvuvi, Uendelezaji wa Misitu, Viwanda, Mawasiliano na usafirishaji, Utalii n.k
Wakichangia kupitia yatokanayo ya kikao kilichopita, wajumbe wa Kikao hicho wameonyesha wapo tayari kufanya uwekezaji kwenye maeneo yaliyotengwa na waliomba watendaji waharakishe michoro na upimaji wa maeneo hayo ili shughuli za uwekezaji zifanyike kwa wakati.
Katika kikao hicho pia Wafanabiashara kupitia chama chao cha TCCIA (TANZANIA CHAMBER OF COMMERCE, INDUSTRY AND AGRICULTURE) waliweza kuelezea baadhi ya changamoto zao ambazo zinakwamisha au kupunguza kasi ya uwekezaji. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na Kushuka kwa bei za mazao hadi kufikia 30% hususani zao la Mahindi ukilinganisha na bei ya mwaka 2017 , Kupanda kwa bei za bidhaa za viwandani hasa Pembejeo za kilimo, Kuchelewasha upimaji wa maeneo ya uwekezaji, na changamoto kubwa zaidi ni Kukatika katika kwa umeme jambo ambalo linakwamisha shughuli za uzalishaji katika viwanda vilivyopo na kukwamisha juhudi za wanaohitaji kuwekeza kwenye sekta ya viwanda.
“ kwakweli Ndugu Mwenyekiti tatizo la kukatika kwa umeme hapa Mbinga sasa limekuwa ni kubwa mno kiasi kwamba shughuli nzima ya ukoboaji wa kahawa kukwamishwa na ikumbukwe kwamba kahawa ni zao ambalo likikwamishwa katika hatua fulani ya mchakato wake basi ubora wake hushuka kwa kiasi kikubwa…tunaomba uongozi wa TANESCO uangalie namna ya kutatua tatizo hilo hasa kipindi hiki cha Msimu wa Kahawa…” alisema Mjumbe Ndg. Jonas Mbunda Meneja wa Kiwanda cha Kahawa Mbinga.
Moja ya azimio kubwa la kikao hicho ilikuwa ni kwamba Meneja wa TANESCO ahakikishe ameomba kibali maalumu cha kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika unapatikana hasa katika kipindi hiki chote cha msimu.
MBINGA
Sanduku la Barua: P.O.BOX 135
Simu ya Mezani: +225 - 2640664
Mobile: +225 – 2640664
Barua pepe: td@mbingatc.go.tz
Copyright ©2018 MBINGA TOWN COUNCIL . All rights reserved.